Friday 10 April 2015

UKIWA NA VITU HIVI VITATU UTAKUWA NA MAISHA BORA


Maisha ni jinsi unavyoyachukulia mwenyewe. Maisha bora unayaandaa mwenyewe. Kuwa na maisha bora na ya furaha kuna vitu ambavyo unatakiwa kuwa navyo. Vitu hivyo huwezi kuletewa na mtu yeyote isipokuwa wewe mwenyewe. Huhitaji pesa, umaarufu ama madaraka ili uwe na maisha bora na furaha. Simaanishi kwamba pesa, madaraka au umaarufu havihitajiki maishani la hasha, namaanisha kuwa kuwa navyo bila kufanya haya ni ngumu kuwa na maisha bora.
Kubadili vitu unavyoweza kubadili
Kubali usikubali kuna vitu ambavyo unaweza kuvifanya ama kuvibadili maishani, hivi vibadili haraka iwezekanavyo. Usisubiri aje mtu mwingine avibadili kwani mara nyingi vyote vipo ndani uwezo wako. Kubadili tabia zako hakuhitaji usaidizi wa profesa wako wa chuo, bosi wako wala mwenyekiti wako wa mtaa. Je huwezi kubadili tabia yako ya uvivu? Huwezi kubadili tabia yako ya ufujaji wa pesa? Huwezi kuamua kuwa na mafanikio? Huwezi kuwa mwekezaji? Bila shaka tabia hizo na nyinginezo nyingi ziko ndani ya uwezo wako na ukiamua kubadili hakika
utaweza. Acha kufanya watu kuwa waamuzi wa maisha yako. Badili tabia ya ulevi, uzinzi, uongo, uchoyo, uaminifu na hakika utakuwa mtu bora, mwenye maisha bora na furaha tele. Badili maisha yako kuwa bora kwa kubadili unavyoweza kubadili.
Kubali vitu ambavyo huwezi kubadili
Kama tulivyoona hapo juu, kuna vitu ambavyo unaweza kuvibadilisha na ambavyo huwezi kubadilisha. Kubaliana na hali ya ukweli huo na utaisha maisha bora sana. Naomba usichanganye kukubali na kukata tamaa. Mfano kuna watu huwa hawapendi mabadiliko, watu wenye mawazo hasi na vikwazo kubali kuwa huwezi kuwabadilisha kama umeshajaribu kufanya hivyo na ishi maisha yako bila kuwa na ulazima wa kuwatilia maanani. Kubali kwamba kuanza kuna ugumu na kufanikiwa ni safari, kubali pia kuwa kuna nyakati ngumu, kuna vikwazo, kuna kufisilisika kuna kufiwa na kuna kukatishwa tamaa. Kumbuka kuwa huwezi kubali yaliyopita hivyo yasikukoseshe furaha na kuishi maisha ya leo na kupanga vyema ya kesho. Kuna vingi ambavyo kwa hakika huwezi kuvibadili, kubali yaishe na usonge mbele na maisha yako. Kumbuka pia kuwa hutoweza kufanya kila kitu hapa duniani na hivyo wewe jitahidi kufanya kwa nafasi yako na ambavyo hutaweza kuvifanya ama kuvibadili watafanya watu wengine kama anavyotuambia mwandishi Richard Carlson (PhD) katika kitabu chake cha Don't Sweat the Small Stuff ... and it's all small stuff, usiishi kama utaishi milele na kujaribu kufanya kila kitu.
Kuwa na busara ya kutofautisha vitu hivyo viwili
Pia itakulazimu kuwa na busara ya kuvitofautisha vitu hivi viwili, yaani vile ambavyo unavyoweza kuvibadili na ambavyo huwezi kuvibadili. Utawezaje kutofautisha? Sina jibu la moja kwa moja lakini kwa msaada mdogo waweza kwa kuwa karibu na Mungu, kusoma vitabu na kukaa na watu wenye busara na waliofanikiwa. Hizi na nyinginezo zinaweza kukusaidia. Katika kitabu cha Tough times never last, but tough people do kilichoandikwa na Robert H. Schuller (Nyakati ngumu hazidumu lakini watu imara hudumu) mwandishi amesema kwamba likitokea jambo lolote, la kwanza unalotakiwa kulifanya ni kuwaza. Hivyo basi inatakiwa uwaze ili uweze kupata busara hizo.waza kabla ya kutenda usije kuacha kubadili jambo ambalo unaweza kulibadili na kung’ang’ania jambo lililo juu ya uwezo wako.
Asante kwa kusoma Makala yahii. Karibu kwa ushauri, maoni na mapendekezo.
Unaweza pia kulike blog hii facebook kwa kusearch: Life Adventures, kufollow twitter kwa @johnicky08 na google plus kwa; Nickson Yohanes.

0 comments:

Post a Comment

Note: only a member of this blog may post a comment.