Wednesday, 3 December 2014

Madhara ya kuwa mdaiwa sugu



Katika maisha huwezi kupata kila kitu unachokitaka, pia huwezi kuhitaji kila unachokipata. Hakuna mtu yeyote duniani ambaye amejitosheleza kwa kila kitu na asihitaji msaada wa mtu mwingine yeyote, hata Billgates huhitaji msaada wa watu wengine ili aweze kuishi na kustawi katika maisha na biashara zake. Hakuna mtu yeyote ambaye anaweza kuishi maisha yake yote ya hapa duniani bila kukopa,hivyo basi kukopa sio jambo baya wala la ajabu. Jambo lililo baya ni kuwa mdaiwa sugu ama kutolipa madeni. Watu wengine hushindwa kulipa madeni si kwa sababu hawana uwezo wa kuyalipa bali hawaoni umuhimu ama hujisahau katika hilo.
Lengo la makala hii fupi ni
kujaribu kuelezea madhara hasa yanayotokana na mtu kutolipa,kuchelewesha ama kutopenda kulipa madeni. Kitendo cha mtu kukuamini na kukukopesha ni kutokana na kuwa na imani na wewe. Mathalani ulikuwa na shida ya laki moja asubuhi na ukajaribu kukopa kwa mtu mwenye laki moja na nusu,kutokana na kuamini kuwa utarudisha hela zake katika muda uliomuahidi hatakuwa na wasiwasi wa kukukopesha kwani anajua hutaharibu mipango yake. Kitendo cha mtu kukukopesha kiasi fulani cha pesa ni kutokana na kukuamini tu na si kwamba yeye ana hela nyingi kuliko wewe. Hivyo basi imani kubwa iliyojengeka kwako ni kama shilingi pekee uliyo nayo wakati wa dhiki na ndiyo pekee itakayokusaidia. Binadamu tumekuwa wepesi sana kukopa lakini pia tumekuwa
 wagumu sana kuwalipa wadeni wetu.  Madhara yake yanaweza yasiwe ya muda mfupi ama matunda yake usiyavune mapema lakini ukaja kuyaona baada ya hata miaka mingi kupita.
Madhara yake
Kupoteza uaminifu; kama nilivyoeleza mwanzo, uaminifu ni kama shillingi ya pekee uliyonayo wakati wa shida na usijue sehemu ya kupata nyingine. Mtu asiyependa kulipa madeni au asiyelipa kwa wakati hupata tabu sana pale atakapohitaji kukopa. Hii inasababishwa na sababu kwamba hakuna mtu anaependa kupoteza mali yake/fedha zake. Hivyo basi itamuwia vigumu mtu huyo kupata msaada wa haraka pale itapotokea akaenda kumkopa mtu mtu ambaye ama hakulipa deni lake au alilichelewesha kiasi cha hata wengine kuzipata katika vyombo vya dola. Mathalan nishawahi kumsikia rafiki akisema,Hela hii uliyochukua itakuwa hela yangu ya mwisho kwako.
Kusambaa kwa sifa mbaya; kama usambaavyo moto katika nyasi kavu,ndivyo isambaavyo tabia mbaya ya mtu. Mathalani utasikia kwa jama wanasema``Jamaa huyu bhana halipi madeni,ukimkopesha umeliwa” kauli kama hizi huzuia mianya ya wewe kusaidiwa wakati wa shida na watu wengine amabao wamepata sifa zako mbaya.
Kukosa Amani; huu ni kama ugonjwa, hueweza kusababisha mtu kuwa na hasira,kuhisi kudhalilishwa ama kuona aibu. Hii hutokana na tabia za baadhi ya watu kutokuwa na staha katika kudai madeni yao hali ambayo hupelekea baadhi ya wadai kutoa maneno makali na ya kudhalilsha hata mbele ya watu unaowaheshimu. Na pia hupelekea pia baadhi ya watu kubadlisha njia zao za kawaida katika juhudi zao za kukwepa wadai wao, kutopokea simu wala kujibu barua pepe au hata ujumbe mfupi wa maneno (sms).
Kufilisiwa; baadhi ya watu huchukua hatua zaidi kwa kufilisi wadaiwa wao kitendo ambacho huwapa mzigo baadhi ya ndugu,jamaa au marafiki. Husababisha baadhi ya watu wanaokutegemea kuishi katika dhiki pale unapofilisiwa na mtu binafsi au taasisi za kifedha.
Kuvunjika kwa mahusiano; uhusiano baina ya watu kama marafiki, wachumba na hata ndoa huweza kuvunjika kwa udaiwa sugu. Mfano kitendo cha mtu kukosa uaminifu huweza kusabisha kufa kwa urafiki. Ndoa ama uchumba huweza kuvunjika pale ambapo madeni yamezidi upande mmoja na hakuna juhudi zozote za kulipa.
Kukwaza wanaokudai; kila binadamu huzaliwa ama huwa na tabia yake na hata udhaifu wake. Wengine hawachoki kukudai lakini wapo wale ambao kwao hilo ni kama zigo la misumari ,huhitaji pesa zao ili kutumiza mahitaji yao lakini huhisi kama kukudai ni kama kukudhalilisha. Wengine watashindwa hata kukushitaki, kukudai kwa jinsi yoyote mpaka ile siku utakayoona vyema kulipa deni lako.
Mauaji; mauaji huweza kutokea pale mdai anapoona kwamba hakuna jinsi yoyote ambayo yeye anaweza kupata haki yake na kuamua kuchukua uhai wa mdaiwa. Pia watu wengine huamua kujiua kwa kukwepa fedheha ya kudaiwa.
Kupoteza fursa zingine (deals); hakuna jambo baya maishani kama kukosa ama kupoteza fursa (missing opportunity). Hii hutokana na madaiwa kujijengea tabia ya kutopokea ama kujibu simu,barua pepe au ujumbe mfupi ambao waweza kutoka kwenye namba mpya ama anuani mpya au hata anoyoijua. Pia mdai anaweza kupata fursa ambayo anaweza kumpa mdaiwa,lakini kutokana na kupoteza imani,kuwa na kinyongo kwako ama kuharibika kwa uhusiano kati yenu akashindwa kukushirikisha.

Asante kwa kusoma makala hii, kwa ushauri, maoni au nyongeza usisite kuwasilisha.

0 comments:

Post a Comment

Note: only a member of this blog may post a comment.