Monday 30 March 2015

Kanuni za uongozi bora


Uongozi ni kuonyesha njia kwa wengine. Uongozi thabiti huweza kushinda nyakati ngumu katika hii dunia, huku uongozi mbovu ukiitumbukiza jamii katika majanga na majuto. Dunia hii ishawahi kuwa na viongozi bora sana. Je unamkumbuka Abraham Lincoln, Mwl J.K. Nyerere, Sokoine, Mandela na wengi wengineo ambao wamekuwa mfano wa kuigwa vizazi kwa vizazi. Najua kuna wabovu pia ambao unawafahamu kuanzia ulimwengu wa kwanza mpaka wa tatu. Hayati Dr. Myles Munroe aliwahi kusema ‘jeshi la kondoo linaloongozwa na simba ni rahisi kulishinda kundi la simba linaloongozwa na kondoo’. Maana yake
ni kwamba mafanikio ya kundi fulani hutegemea sana kiongozi anayewaongoza.
   1. Upo katika roho ya kila binadamu
Kila binadamu kiasili ameumbiwa uongozi. Kila mtu huzaliwa kiongozi. Lakini kwanini si kila mtu anakuwa kiongozi katika maisha yake? Jibu ni moja tu mazingira hayakumjenga yeye kuwa kiongozi. Wewe kuwa kiongozi ni maamuzi na utashi wako tu. Kwani kama mazingira hayaruhusu yabidi ubadili mazingira au ujibadili mwenyewe. Kuwa kiongozi au mfuasi ni chaguo lako.
   2. Uongozi haufundishi bali hugunduliwa
Katika hotuba yake aliyowahi kuitoa hayati Dr. Myles Munroe iitwayo ‘10 attitudes of leadership’, alisema kwamba uongozi upo kwa kila mtu na hivyo la muhimu ni kugundua kipaji hicho ambacho kiko ndani ya mtu. Huwezi kusema ardhi hii haina madini wakati bado hujafanya uchunguzi. Serikali, mashirika na makampuni mbalimbali wamekuwa wakiwapeleka wafanyakazi wao katika vyuo, warsha na makongamano mbalimbali ili kujifunza uongozi. Lakini ukweli ni kwamba wanarudi bila kitu kama hawajaweza kwanza kufanya ugunduzi uliopo ndani yao.
   3. Uongozi hugunduliwa na mtu binafsi
Kama nilivyosema katika pointi iliyotangulia ni lazima kwanza ugundue kuwa wewe ni kiongozi kutoka ndani. Kushindwa kugundua ni sawa na kuchagua kuwa mfuasi na sio kiongozi. Una uwezo wa kuwa kiongozi na kufikiri kama kiongozi lakini kuwa mfuasi wa kiongozi fulani ni chaguo lako mwenyewe na hakuna wa kumlaumu popote duniani.
   4. Kutumia kipaji chako kuhudumia wengine
Kila mtu huzaliwa na kipaji chake, wengine huwa na zaidi ya kimoja. Usijaribu kuviendeleza vyote bali tafuta kimoja cha kukikuza. Ukijaribu kukuza vyote kwa pamoja unaweza kuvipoteza vyote. Kuza kimoja baada kingine. Kipaji cha uongozi kipo kwaajili ya kutumikia ama kuhudumia wengine. Kadiri unavyohudumia watu ndivyo unavyokuwa kiongozi bora. Umepewa kipaji kutumikia watu kwani kipaji ulichonacho kina thamani ndiyo maana umepewa na watu wanakithamini. Kuhudumia wengine ni wajibu wako. Yesu Kristo aliwahi kusema anayejiona mkuu kuliko wote na awatumikie wengine’ kama huwezi kuwahudumia watu hufai kuwa kiongozi. Hupaswi kuogopwa na watu bali kuheshimiwa nao na pia hupaswi kuabudiwa kama Mungu. Gundua kipaji chako na usijaribu kudandia kipaji cha mtu mwingine kwani hutofika popote.


    5. Uongozi ni kujitegemea (deployment)
Hakuna mtu atakayeweza kuwa huru kama kiuchumi hayupo huru. Mtu asiyejitegemea kwa mapato hawezi kuwa kiongozi bora hata siku moja. Je mtumwa anaweza kuwa kiongozi wa mabwana zake? Jibu ni hapana. Kiongozi anapaswa kuwa kuwa muajiri na siyo mwajiriwa kwani akiwa mwajiriwa atakosa uhuru wa kufanya maamuzi. Mfumo wa elimu kote duniani hufundisha watu kuwa wataalamu na kupata kazi nzuri. Mfumo haufundishi watu kuwa wawekezaji au wafanyabiashara. Kuajiriwa hakutakufanya kuwa kiongozi bora. Kama unataka kuwa kiongozi anza na kujitgemea kiuchumi. Ulifundushwa kuwa mwajiriwa lakini kizuri zaidi ni kuwa unaweza pia kujifunza kujitegemea na kusahau kuhusu kuajiriwa. Chukulia ajira yako ya sasa kama ni ya muda tu ni si ya kudumu
    6. Kuwa dhahiri
Utakuwa kiongozi tu pale utakapojigundua kuwa kiongozi na kuamua kuwa kiongozi. Uongozi upo ndani ya nafsi yako. Andaa mazingira yako vizuri kwani yanaweza kuwa kikwazo chako kikubwa katika kukuza kipaji chako cha uongozi. Kiongozi lazima ufanye vitu ambavyo ni vigumu kuvilipa. Kiongozi lazima uweze kuthubutu. Kama huwezi kuthubutu basi hufai kuwa kiongozi.
   7. Kujitokeza/Exposure
Uongozi bora ni ule ambao kiongozi amejitokeza na kujulikana kwa watu. Sera na vitu ambavyo anavisimamia na kuamini pia vijulikane. Kama mtu hana dira hawezi kuwa kiongozi mzuri kwani ni sawa na kutokujua anapokwenda. Atawezaje kuongoza watu kama mwenyewe hajui anapokwenda?
Asante kwa muda wako. Tukutane katika makala nyingine ya uongozi.

0 comments:

Post a Comment

Note: only a member of this blog may post a comment.