Wednesday 18 March 2015

Umuhimu wa kuwa na marafiki


Pengine unaweza kujiulliza ni kwaninini nimeamua kuandika kuhusu umuhimu wa marafiki. Lakini mbali na hilo nikuulize una rafiki?  Najua unalijua jibu lako, lakini nisingependa uniambie. Najua kwamba unajua umuhimu wa marafiki ila nimeona nikukumbushe tu. Marafiki ni tunu kubwa tuliyonayo hapa duniani. Marafiki wanaweza kuwa chanzo cha wewe kufanikiwa ama kuporomoka katika nyanja mbalimbali. Kuna aina mbili za marafiki ambazo nitazitaja ni hapa ambazo ni urafiki wa karibu (close friends) na urafiki wa kawaida (acquaintances). Labda nianze na urafiki wa kawaida. Urafiki wa kawaida ni ule ambao mmekutana sehemu kama baa, kwenye michezo, muziki, sherehe au katika siasa na pia kwenye mitandao ya kijamii kama facebook. Urafiki huu hutokana na nyie kuunganishwa na kitu fulani. Mara nyingi urafiki huu ni wa muda tu na unaweza kuisha pale tu ambapo mtapoteza kile kitu kinachowaunganisha (common interest). Lakini aina ya pili ya urafiki ni ule urafiki wa karibu ambao unakuwa karibu na mtu,
mnasaidiana katika hali zote, mnavumiliana katika madhaifu yenu, mnaweza kushirikiana siri zenu za ndani kabisa na kuaminiana pia. Urafiki huu unaweza kuvuka mipaka na kuwa kama undugu. Urafiki huu ni wa kudumu na ndio ninaoulenga hasa katika makala hii fupi. Karibu tuzunguke pamoja katika Life Adventures.
 1. Hukuletea furaha
Kumuona tu rafiki yako wa dhati huweza kubadili hali yako ya huzuni kuwa furaha. Mtakumbushana ya kale, mtajadili ustawi wenu na hata matatizo yenu. Atakufariji na pia atashirikiana na wewe bega kwa bega katika kuhakikisha urafiki wenu unamea na kudumu katika ustawi wa hali ya juu. Haya na mengine mengi yatastawisha furaha yako.
 2.  Hukusaidia kufikia malengo yako
Rafiki hukusaidia wewe kutimiza malengo na ndoto zako. Hukupa ushauri bora, hukusaidia kwa hali na mali na hata kukutia moyo katika nyakati ngumu. Pia rafiki hukusaidia kuacha tabia mbaya na hatarishi kama ulevi, utumiaji dawa za kulevya, uzinzi, uasherati na mengine yanayofanana na hayo.  Hamasa/faraja ya rafiki yako ni kama mbolea katika mmea.
 3.  Ni msaada mkubwa uzeeni
Katika umri mkubwa watu wengi hupitia nyakati ngumu kama kustaafu, magonjwa na hata kupoteza wapendwa wao. Usipokuwa na rafiki wa kukutia moyo unaweza ukadhani dunia imekutenga. Kuwa na marafiki kutakusaidia uweze kuyashinda yote na kuona maisha katika mwanga mpya. Utaishi mwenye matumaini mapya na makubwa. Utaishi maisha yenye furaha na kuongeza siku za kuishi pia.
 4. Hupunguza msongo wa mawazo na kukata tamaa
Kuna wakati katika maisha ambapo watu huona kama dunia imewaelemea. Hukumbwa na msongo wa mawazo na kukata tamaa. Wengine hushindwa na hali  na kupelekea kujiua wakidhani ni suluhisho, la hasha. Watu wengi wanaochukua hatua hii ni wale wenye uhaba wa marafiki ama hawawaamini marafiki zao. Wanasaikolojia husema kwamba kueleza tatizo lako kwa mtu unaemuamini husaidia sana kwa kiasi kikubwa na hupunguza mzigo mkubwa moyoni na pia kulitatua kwa nusu.  Marafiki hukufariji, hukutia moyo na pia hukupa njia mpya za kutatua tatizo lako.
 5. Ni msaada kwenye nyakati ngumu
Kuna watu walishawahi kusema matatizo tumeumbiwa binadamu, lakini pia waandishi wengi wa vitabu wanasema changamoto/matatizo hubeba fursa ndani yake. Lengo hasa ni wewe kutoona kama matatizo ni yako peke yako na hayana suluhisho. Si lengo langu hasa kukujuza hilo lakini nalo ni muhimu kulifahamu. Kuna wakati binadamu hukabiliwa na nyakati ngumu mfano ukata, magonjwa, msongo, kufilisika,kufukuzwa kazi kufungwa jela na hata kupoteza wapendwa wao. Kumuona rafiki akikusaidia hufariji sana. Lakini pia wamekuwa watu wa muhimu katika maisha yetu hasa katika nyakati ngumu. Marafiki wamesaidia wenzao kulipa karo za shule, kuuguza, kutoa mtaji, msaada wa kisheria, chakula na misaada mingine mingi ambayo sitaweza kuitaja yote hapa. Naamini baada ya hapa utatafuta rafiki wa karibu kama huna, na kwa wewe uliye naye jitahidi kumlinda kama mboni ya jicho.
Asante kwa kuniazima muda wako kusoma makala hii. Tukutane katika makala nyingine, wakati mwigine. Kwaheri.

0 comments:

Post a Comment

Note: only a member of this blog may post a comment.