Tuesday 12 May 2015

Hizi ndizo kanuni za kuwa na afya njema

Ili uweze kufanya shughuli zako za kila siku ikiwa ni pamoja na shughuli za uzalishaji mali ni lazima uwe na afya njema. Afya ni hali ya kuwa vizuri kimwili, kiakili, kisaikolojia na kiroho pia. Watu wengi huchukulia kuwa watu wanene ndio wenye afya njema na wakati mwingine hudhani kuwa watu wembamba ndio wenye afya. Lakini kiukweli hilo si kweli.  Mtu mwenye afya ni yule mwenye sifa nilizotaja hapo juu.

Kama huna mojawapo kati ya hivi basi hatuwezi kusema kuwa una afya njema. Ukiwa na afya njema utaweza kuishi maisha yenye furaha na amani na pia utaweza kujizalishia kipato chako kwa kila siku iendayo kwa Mungu. Ili uwe na afya njema inakupasa
ufanye yafuatayo kila siku kama siyo kila mara. SOMAHizi ndizo kanuni za kuwa na afya njema
  1. Kula vizuri/kula mlo bora
Ili uwe na afya au siha njema kama binadamu inakubidi ule vizuri kila siku. Mlo bora si lazima uwe na nyama kila siku kama wengi wanavyodhani. Sio lazima ule mlo mkubwa sana bali ule chakula cha kukutosha kila siku. Lazima ule mlo wa kukutosha na si kula chakula kisichojitosheleza. Kula sana matunda na mboga za majani kila siku ili uweze kuboresha afya yako. Epuka kuwa na mwili mkubwa kupitiliza kwa hiyo pia kula kulingana na uzito wa mwili wako. Kumbuka kama hutaweza kula chakula bora kama dawa kwa sasa basi unajiandaa kula madawa baadae kama chakula. Madhara ya kula vibaya unaweza usiyaone sasa hivi bali kwa muda mrefu ujao.
man eating healthy
  2. Fanya mazoezi ya viungo kila mara
Nakushauri kila siku ufanye mazoezi ya viungo. Kama ratiba imekubana unaweza kutenga siku kadhaa katika wiki ambazo utatumia kwa mazoezi, pia unaweza kutenga muda mfupi sana wa hata dakika kumi kila siku. Naamini katika saa 24 za siku huwezi kukosa angalau dakika kumi za kufanya mazoezi. Faida ya kufanya mazoezi ni kama kuongeza msukumo wa damu mwilini, kusaidia katika mmeng’enyo w achakula, akili kufanya kazi vizuri, kupata usingizi mzuri na kadhali. Unaweza kufanya mazoezi mepesi kila siku kama kukimbia, kuruka kamba na push-ups. Mwanzo utaonekana mgumu lakini kadiri siku zitakavyoenda utazoea na utakuwa huwezi kukaa bila kufanya mazoezi. Kumbuka mazoezi husaidia wewe kuwa na nguvu na afya bora katika umri wowote.
  3. Pata usingizi wa kutosha
Katika siku yenye saa 24 tenga muda wa kutosha wa kuweza kupata usingizi. Jitahidi ulale kwa angalau saa 7 hadi 8 kwa siku kama inavyoshauriwa na wataalamu. Hii itakujengea afya ya akili na afya ya mwili pia. Utafiti uliofanywa unaonyesha kuwa watu wanaopata usingizi wa kutosha kila siku hufanya kazi zao vizuri kulinganisha na wale wasiopata usingizi wa kutosha. Kumbuka mwili wako sio roboti hivyo kulala ni sehemu ya maisha yako. Hutaweza kumaliza kila kitu kwa kutokulala. Kama wewe ni mwanafunzi na umebanwa na ratiba za shule tenga muda wa kufanya mambo yako ya msingi na kuachana na visivyo na msingi kwako. Kama unaingia zamu ya usiku kazini kwako, basi tenga muda wa mchana kupumzika.
  4. Kunywa maji ya kutosha kila siku
Jenga mazoea ya kunywa maji kila siku. Kunywa maji safi na ya kutosha kila siku. Usisubiri mpaka uhisi kiu. Nakushauru unywe maji safi kwani maji ambayo siyo safi na salama huambukiza magonjwa kama kipindupindu, kuhara, taifod n.k. maji yana faida nyingi mwili kama kupoza mwili kwenye joto, usafirishaji mwilini, kusafisha mwili kama figo n.k. Ukosefu wa maji mwili una hasara nyingi kuliko faida. Hakuna kinywaji kinachoweza kuchukua nafasi ya maji, hivyo basi kaa ukijua kwamba maji yana umuhimu wa kipekee mwilini na ndio maana zaidi ya robo tatu ya mwili wako ni maji. Hata kama unapenda unapenda soda au chai usiache kunywa maji kila siku.
  5. Punguza msongo wa mawazo
Msongo wa mawazo ni hali ya akili kulemewa na mawazo mengi bila kuwa na namna ya kufanya utatuzi. Kama hali ikikutokea haina maana kwamba ndiyo unatatua tatizo bali unaongeza tatizo kwani hutaipa akili kufikiria namna ya kutafuta ufumbuzi. Kaa chini fikiria uwezekano wa kutatua tatizo lako, omba msaada kwa watu wako, mwambie ndugu au rafiki unaemuamini na pia nenda sehemu nzuri kuweza kupunguza mawazo. Kadiri unavyokuwa na mawazo ndivyo unavyozidi kuharibu afya yako. Kama huna afya ya saikolojia basi huna afya kwani mwili wako unaitegemea akili yako kuweza kufanya kazi. Acha kuangalia matatizo yako bali ona kama changamoto na pia tafuta namna ya kuweza kufanya utatuzi. SOMA Causes effects and management of stress
  6. Usitumie vilevi au madawa ya kulevya
Nakushauri kama unatumia sana vile punguza au acha kabisa. Kama unakunywa kidogo kama sehemu ya burudani sio mbaya ila kama unakunywa kama sehemu ya kukimbia matatizo yako basi nakushauri uache mara moja kwani tatizo halikimbiwi bali hutatuliwa. Kuna watu wmekuwa wakitumia vilevi na madawa ya kulevya kama sehemu ya maisha yako na sehemu ya burudani. Kama unalewa mpaka unashindwa kujitambua unapata faida gani hapo? Unapoteza pesa,unaharibu afya, unaharibu mahusiano na pia unajipotezea heshima mbele za watu. Kwa upande wa madawa ya kulevya achana nayo kabisa kwani hakuna faida yoyote unayoipata zaidi ya starehe ya dakika chache ambayo itakuacha ukiwa teja usiyekuwa na mwelekeo.

 Madawa kama bangi, kokein, heroin n.k. Hata sigara kaa nayo mbali. Unaharibu afya ya akili yako na hata afya ya mwili wako, unashindwa kuzalisha mali na pia unajiandalia mazingira ya kuugua saratani hasa unapotumia sigara.
  7. Pata muda wa kupumzika
Kama nilivyosema hapo juu wewe ni binadamu, kiumbe ambaye unachoka. Mashine zinachoka na kupumzika sembuse wewe mwanadamu? Tenga muda wa kupumzika na kutafakari maisha yako. Upe mwili nafasi ya kuweza kujijenga upya na kupata nguvu mpya. Ila sikushauri upumzike kupitiza kwani huo utakuwa ni uvivu. Kupumzika baada ya kazi ni vizuri lakini kupumzika kabla au ukiwa hujafanya kazi ni uvivu. Muda ambao wewe utaupanga kupumzika ni juu yako mwenyewe kuamua. Kumbuka katika kipindi cha kuupumzisha mwili wako ndipo na mawazo mapya na ya kujenga huja.
  8. Kuwa na furaha na acha uoga
Hakuna siku ambayo utapanga kuwa na furaha zaidi ya leo. Jana ni siku ambayo ilishapita na haitarudi tena katika maisha yako yote hivyo kwa vyovyote isikuaharibie siku njema ya leo. Kesho nayo ni siku usiyokuwa na uhakika nayo kwa hiyo isikuharibie leo yako. Leo ndio siku ambayo unatakiwa uwe na furaha na ufurahi kwa kila siku iitwayo leo. Matatizo yasiwe sehemu ya kukuibia furaha yako. Pia usijiwekee vigezo kwamba nitakuwa na furaha pale nitakapofanikisha kitu fulani.  Pia acha woga kwani utaharibu maisha na mafanikio yako. Kabiliana na kila tatizo kwa tumaini kubwa kwani kila tatizo huja na namna yake ya kutatuliwa. Mwisho jua kuwa kama maisha yako hayana furaha na amani yatakuwa maisha yasiyo na thamani.
Natumaini umejifunza misingi ya afya bora. Najua kuna vitu vingi kuhusu afya ambavyo sijaandika, natumaini utaendelea kujifunza zaidi ili uwe na afya njema. Kumbuka afya ndiyo msingi na kipaumbele cha kwanza katika mafanikio yako

Kwa maoni, ushauri au mapendekezo usisite kuwasiliana nami kwa e-mail: nmyohanes@gmail.com au kwa simu namba 0712-843030.

2 comments:

Unknown said...

asante kwa ushauri ubarikiwe sana!

Unknown said...

ahsante mr

Post a Comment

Note: only a member of this blog may post a comment.